Usalama wa kimazingira, wa kihisia na wa kidijitali kwa watetezi wa haki za binadamu wanaofanyia kazi za kiofisi majumbani kwao katika kipindi hiki cha mlipuko wa Virusi vya Corona (COVID-19)
Dondoo na vidokezo kwa Watetezi wa Haki za Binadamu
Tafadhali tutumie mawazo au mapendekezo yako kuhusu usalama kulingana na uzoefu wako ambayo unadhani yatawasaidia Watetezi wengine wa Haki za Binadamu au Mashirika yanayotetea Haki za Binadamu kujikinga dhidi ya maambukizi. Pia tutaendelea kuuboresha mwongozo huu.
(* Mwongozo huu umetafsiriwa kutoka lugha ya Kiingereza kwenda lugha ya Kiswahili kwa hisani ya Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) ili utumiwe na Watetezi wa Haki za Binadamu au Mashirika yanayotetea Haki za Binadamu yanayotumia lugha ya Kiswahili.)
Mlipuko wa gonjwa hili duniani ni jambo jipya kwetu sote. Wengi wetu tumelazimika au tutalazimika kufanyia kazi zetu mbali na ofisi. Wengi watatumia nyumba zao kama ofisi. Kwenye baadhi ya maeneo, bila shaka janga hili litatumika kuminya haki za Watetezi wa Haki za Binadamu na Mashirika yanayotetea Haki za Binadamu kama ambavyo imewahi kutokea katika vipindi vya nyuma. Mazingira na hisia zetu zinatofautiana kwa kila mmoja wetu.
Hata hivyo, Front Line Defenders ina uzoefu wa kuwashauri Watetezi wa Haki za Binadamu wanaofanyia kazi zao mbali na ofisi, na hata baadhi ya wafanyakazi wetu -kwa miaka mingi sasa- wamekuwa wakifanyia kazi zao za kiofisi wakiwa majumbani kwao huku wakiwa salama. Yafuatayo ni mawazo na mambo tuliyojifunza kuhusu changamoto za mfumo huu wa utendaji kazi. Hata hivyo, si rahisi kuwa na suluhu ya kila changamoto itayomfaa kila mmoja, hususani kuhusu usalama wa kihisia na kimazingira. Hii ni kama motisha ya kukusiadia kutathmini na kuboresha usalama wako kulingana na hali yako uliyonayo. Na kama wewe ni Mtetezi wa Haki za Binadamu au Shirika linalotetea Haki za Binadamu ambalo liko kwenye hali ya hatari nchini mwako, unaweza kuwasiliana na Front Line Defenders kwa msaada zaidi – kwa kuwa tupo kazini muda wote hasa katika kipindi hiki.
Pia tunashauri mwasiliane haraka na kwa uwazi na wafadhili na wadau wenu kuhusu mazingira yenu ya kazi kwa sasa. Wafadhili wa masuala ya haki za binadamu wanaelewa uhalisia wa changamoto za janga hili kwa wadau wao pamoja na wanufaika wa ufadhili wao. Tunaamini wakifahamu kazi zinazowezekana na zipi haziwezekani kufanywa na shirika lako, pamoja na uhusiano wenu katika kipindi hiki, iwatasaidia kukabiliana na hali iliyopo kwa usahihi zaidi. Pia wafadhili wanaweza kulisaidia shirika kuwapatia wafanyakazi wake mahitaji binafsi kama vile vitendea kazi vya kufanyia kazi nyumbani au pengine kuimarisha zaidi usalama wa wafanyakazi wakiwa majumbani.
Usalama wa Kimazingira
Tafadhali zingatia eneo au chumba salama cha kufanyia kazi zako nyeti au za siri. Kwa mfano; Je kufanyia kazi chumba cha chini (basement) ni salama zaidi? Je ni rahisi mvamizi kuingia chumba unachofanyia kazi bila vizuizi vyovyote au milango kwenye nyumba yako? Je, watu wa nje wanaweza kuona mwanga wa kompyuta yako kwenye dirisha lako wakati unafanya kazi hasa nyakati za usiku? Je, unaweza kuwazuia unaoishia nao nyumbani kuona kazi unazofanya? Au kuwazuia kusikia mazungumzo yako ya siri unapoongea na simu au uwapo mtandaoni? Unaweza kuongea kwa sauti ya chini endapo unahofia majirani wanaweza kusikia mazungumzo yako, funga madirisha ukiwa unazungumza au tumia lugha ambayo wengine hawawezi kuelewa.
Usiache vifaa vyako vya kazi maeneo ya wazi nyumbani (mfano USB na dokyumenti mbalimbali). Kuwa na mpangilio na linda taarifa nyeti. Tafuta kufuli na ufungie vifaa vyako kwenye kabati. Tafuta pia sehemu salama za kufichia vitu vyenye taarifa nyeti. Kuwa mbunifu, kwa mfano, unaweza kuficha vitu vyako chini ya tofali au kigae au ukutani au darini, na kadhalika (n.k).
Kila mwisho wa siku, tunza kila kitu chako mahali salama ikiwa ni pamoja na dokyumenti zote, kompyuta na simu. Kuwa na tabia ya kusafisha meza yako ya kazi. Zima kumpyuta yako na usiiache ikiwaka.
Weka utaratibu wa kuharibu taarifa nyeti na mafaili. Mfano, unaweza kuzichoma, kuzichanachana n.k.
Zingatia kutumia mifumo rahisi ya kuchunguza eneo unalofanyia kazi nyakati ambazo haupo. Hizi zinaweza kusaidia kujua kama kuna mtu aliingia kwenye chumba chako au la. Waweza kuweka mitego kugundua kama kuna mtu mwingine aliingia nyumbani kwako au chumbani mwako au kufungua droo yako. Hali kadhalika, waweza kutumia njia za kidijitali kwa kutumia simu-janja yako kama programu ya Haven app ambayo unaweza kuipakua mtandaoni.
Hakikisha unafanyia kazi zako mahali panapofaa na umeketi mkao sahihi.
ili usiumie mgongo, shingo au sehemu yoyote ingine ya mwili wako – pata mapumziko mafupi kila baada ya muda fulani. Epuka ajali ndogondogo kama kuteleza na kuanguka. Hakikisha unakuwa na visanduku vyenye vifaa vya huduma ya kwanza. Hakikisha una maji ya kutosha kudumu kwa siku nne pamoja na mahitaji mengine.
Kama unaishi na watu wengine (familia, marafiki), waelimishe ili wazingatie kanuni zako za usalama utazokuwa ukizitumia nyumbani (kama vile kutokufungua mlango/geti bila kujua anayebisha hodi, kutokushika kompyuta yako n.k). Ni muhimu kuitisha kikao cha familia kila siku ili kujua hali ya usalama wa nyumba inaendeleaje na kama wamegundua kitu kipya au wanahisi hali ya hatari.
Andika namba za dharura kwenye vikaratasi na uvibandike ukutani, ama hifadhi kwenye simu au kwenye pochi yako. Zingatia kuwa na mpango wa mawasiliano wa ndani ya nyumba endapo utahitaji msaada. Ikitokea dharura uwapigie wenzako simu na wao watajua nani wa kumpigia kupata msaada na jinsi ya kukusaidia kwa muda huo.
Kuwa na mpango kamili wa kutoroka ndani ya nyumba endapo dharura itatokea, weka milango mingi ya kutokea na mahali pa kukutani mkishatoka nje. Ni muhimu kuufanyia mazoezi mpango wako mara kwa mara kwa pamoja ili muweze kuuzoea. Wakati mwingine kitendo cha kuegesha tu ngazi karibu na fensi yako, kunaweza kuboresha ulinzi nyumbani kwako. Muda wowote unaweza kupanda ngazi na kutoka. Watu wengine huandaa begi la kutorokea lenye vitu vya kuondoka navyo ikitokea dharura na huliweka karibu na mlango wa kutorokea, Ndani ya begi huweka dokyumenti nyeti, fedha, chaja ya simu, tochi, dawa na mahitaji mengine.
Ikiwa kama Mtetezi wa Haki za Binadamu unahisi hali ya hatari eneo unaloishi inazidi kuwa mbaya na itakulazimu kuhama, upitie tena mpango ulioupanga kwaajili ya kuhama. Je, taratibu za safari na kufika huko uendako bado zinawezekana? Je, unawezaje kuutumia mpango wako kuepuka kuonekana na watu ukihama?
Kama unatarajia kukutana na wageni muhimu nyumbani kwako, kuwa makini na zingatia maelekezo ya wataalamu wa afya kuhusiana na tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona. Andaa maelezo ya kuwapa majirani zako endapo watakuuliza kwanini umetembelewa na wageni; ikiwa eneo lenu lipo kwenye karantini. Pia ni vema wageni wako kutowaambia madereva taxi mahali unapoishi. Wanapaswa kuwaambia wawashushie kwenye eneo linalofahamika karibu na unapoishi kama vile duka, kanisa n.k. Na kama wageni wako hutumia usafiri wao binafsi, ni vyema wasishukie karibu na nyumba yako - wanaweza kupaki mbali kidogo na unapoishi ili watu wasijue kama wanakuja nyumbani kwako. Zingatia kuwapa maelekezo sahihi wageni wako ili wasije kumuuliza mtu mwingine njiani jinsi ya kufika kwako.
Muda wote nyumbani kuwa makini na hatari za kiusalama kama moto. Kwa kuwa utakuwa ukipikia ndani zaidi, ukitumia vifaa vingi vya umeme, au pengine kuvutia sigara ndani, watoto nao watakaa ndani sana kwa kipindi hiki, na majirani zako watakuwa majumbani mwao muda mwingi, ni vema kuzingatia kuwa hali hii inaweza kuongeza hatari ya ajali za moto kutokea nyumbani kwako au kwa majirani zako. Hakikisha una mpango mkakati wa kuzima moto.
Kuwa na vifaa vya kuzimia moto kama kutumia blanketi la kawaida kuzimia moto, kuwa na vifaa vya kugundua kama kuna moshi ndani, punguza matumizi makubwa ya umeme, punguza matumizi ya mafuta mengi n.k.
Kaa na alamu binafsi au filimbi nyumbani na ukitoka, tembea nayo ili ikusaidie kupata msaada wa haraka utakapouhitaji endapo utapata dharura njiani.
Muda wote hakikisha milango yote ya nyumba imefungwa, kwa kutumia funguo. Tunza ufunguo mahali tofauti na mlangoni tayari kutumika wakati wa dharura. Tambua njia ambazo wahalifu hutumia maeneo unayoishi. Uwepo wa watu wengi majumbani mwao katika kipindi hiki hupunguza uvamizi majumbani lakini wakati huohuo wizi wa madukani au maofisini unaweza kuongezeka. Hakikisha unaondoka na taarifa nyeti ofisini kwenda nazo nyumbani. Zingatia kuwa katika kipindi hiki maadui zako watajaribu kutumia hii fursa kutokana na wewe kufanyia kazi nyumbani.
Epuka tabia za mazoea hasa unapotoka nyumbani ama uwapo safarini. Kabla hujatoka nyumbani kwako kwenda dukani, zingatia hatari ya kuacha vifaa vyako vya kidijitali (simu na kompyuta) nyumbani dhidi ya kuondoka navyo. Kabla ya kutoka, tafadhali zingatia kuzima vifaa vyako na uvifiche. Unapotoka, hakikisha kuna mtu anayejua unakoenda, utafikaje huko (njia utakayotumia), ni wakati gani unatarajia kurudi tena nyumbani, jinsi ya kuwasiliana na wewe ikiwa kuna haja hiyo, n.k. Pia kupitia simu-janja yako, waweza kuwajulisha watu wako wa karibu mahali utapokuwa kwa muda huo (live location sharing), na kuweka utaratibu wa kuwa unatuma jumbe fupi za kutoa taarifa za mizunguko yako, mfano ("nimefika", "naondoka", "nitakuwa hapo ndani ya dakika 20", n.k.
Tumia busara, epuka kulengwa na polisi au vikosi vya usalama kwa kukiuka sheria zozote za eneo lako katika kipindi hiki.
Ni rahisi kusema kuliko kutenda, lakini kwa sasa, jaribu kujipanga kuichumi kukabiliana na hali hii endapo itaendelea kwa muda mrefu zaidi ya inavyotarajiwa. Ikiwezekana jadili hili swala na wafadhili au wadau wako. Jaribu kuunda mfuko wa dharura wa shirika lako, aidha pekeyako ama kwa kushirikiana na wengine. Wasiliana na jamii kwa njia ya mtandao ili kutambua ni mikakati gani itawanufaisha nyote kwa pamoja.
ULINZI WA KIHISIA
N i muhimu kutambua wewe binafsi pamoja na watu unaofanya nao kazi kwamba, hali hii italeta athari kubwa za kihisia na kisaikolojia. Ni dhahiri kwamba, viwango vya utendaji kazi vitabadilika, na watu watalazimika kuyazoea mazingira yao mapya ya majumbani kuweza kufanya kazi zao za kiofisi, kila mmoja kwa kasi yake mwenyewe. Pia kila mmoja atahisi athari za upweke na kupungua ama kutokuwepo kabisa kwa mawasiliano ya moja kwa moja na wafanyakazi wenzake kama ilivyozeleka awali.
Kwa kipindi hiki, ikiwezekana, pata mtu wa karibu atayekuwa anakuliwaza kuhusu hali yako ya sasa, ambaye utakuwa ukimshirikisha mawazo na hisia zako. Mtu huyo anaweza kuwa mtu ambaye unamuamini na uhusiano mzuri na yeye. Kumbuka, kuwa hali hii inaweza kukuletea hisia, mihemko na mawazo tofauti. Mahitaji na matendo yako yanaweza kubadilishwa pia na hii hali ya sasa. Hivyo basi, jaribu kutafakari kila jambo kwanza kabla ya kutenda. Jaribu kuwa mvumilivu kidogo na mwenye kujijali.
Ikiwa wewe ni mlezi, basi pangilia majukumu yako yote ya siku vizuri ili usifanye kazi kupindukia. Waweza tayari kuwa na mpango wa kukabiliana na hali hiyo, lakini pia tarajia mabadiliko yoyote. Kuna wakati utalazimika kufupisha muda wako wa kazi au majukumu ya malezi, ili uweze kushughulikia majukumu mengine. Inaweza kuwa ngumu kukabiliana na changamoto hizi, lakini jaribu kutuliza akili, ukubaliane na hali iliyopo ili upate suluhu madhubuti. Jaribu kuwa mbunifu na kujisamehe endapo utashindwa kusimamia majukumu yako yote kikamilifu. Pengine tatizo sio wewe, bali mlundikano wa majukumu upo nje ya uwezo wako. Pia, uwe tayari kuahirisha baadhi ya majukumu yako mengine ya kiofisi ama ya nyumbani.
Hakikisha unakula kiafya zaidi (pamoja na vitafunio!), kwa wakati unaofaa kwako, lala masaa ya kutosha na kwa wakati unaofaa kwako na pia fanya mazoezi ya mwili kila siku. Kumbuka kwamba, uamuzi wa kufanyia kazi za kiofisi ukiwa nyumbani pamoja na hali ya upweke unayoweza kuwa nayo kwa sasa, vinaweza kuendelea kwa muda mrefu zaidi ya ilivyotarajiwa hapo awali.
Kila siku, weka ratiba ya majukumu yako ya siku nzima na uhakikishe unayatimiza kadri uwezavyo. Epuka kuchanganya kazi za kiofisi na shughuli zako kibinafsi. Uwapo nyumbani, tumia wakati wa kufanya kazi za kiofisi kana kwamba upo ofisini. Vivyo hivyo, utumie wakati wa shughuli zako binafsi kama vile ungekuwa mbali na ofisi. Itakusaidia kuweka mipaka ya kazi. Zima kompyuta yako unapomaliza kufanya kazi za kiofisi, au funga programu zako za jumbe fupi na barua pepe n.k.
Ukiweza, panga sehemu moja maalum kwenye nyumba yako itayokuwa eneo lako la kufanyia kazi za kiofisi, kuepuka kufanyia kazi kila mahali ndani ya nyumba. Hii itakufanya uhisi upo kazini. Pia itahakikisha kazi zako za kiofisi haziingiliani na shughuli zako binafsi na kinyume chake. Hii itawaashiria watu unaokaa nao nyumbani, kuheshimu muda unapokuwa umekaa "mahali pa kazi" kwakuwa upo "kazini" na hauitaji usumbufu. Kamwe usifanyie kazi kwenye maeneo ambayo unayatumia kwa ajili ya kupumzika au kula chakula!
Ikiwa hauko kwenye karantini, toka nje kila siku utembee, ukimbie, uendeshe baiskeli, n.k. Unaweza kufanya hivi wakati wowote, lakini ni vema ukawa na utaratibu maalum (kwa mfano: Kufanya matembezi baada ya chakula cha mchana, kukimbia asubuhi kabla ya kuanza kufanya kazi, n.k). Angalau kila baada ya lisaa limoja, simama, jinyooshe, tembeatembea, fumba macho yako kwa muda mfupi kisha uendelee na kazi.
Tafakari jinsi kiwango cha kelele, muziki au sauti ya redio mahali ulipo kinakusaidia kufanya kazi vizuri ama la kukuzidishia msongo wa mawazo na uchovu? Rekebisha hali hiyo kulingana na mahitaji yako (yanayoweza kubadilika kila siku!).
Ili kudhibiti wasiwasi wako, punguza kufuatilia taarifa za kuenea kwa maambukizi ya COVID-19 kila wakati, badala yake, tenga muda maalum wa kufuatilia habari. Usisome habari mida ya jioni wakati unajiandaa kulala. Iwapo utahisi kufadhaika au kuwa na msongo wa mawazo, basi zingatia kufanya na/au kuwasaidia wenzako kufanya shughuli za kudhibiti msongo wa mawazo - kama vile - kutafakari, kufanya mazoezi ya yoga, au kusali.
Ikiwa unaishi na watu wengine nyumbani, hakikisha kila mmoja anapata wakati wa kukaa kimya pekeyake kutafakari au kupumzika, hata kama itakubidi ujifungie pekeyako chooni kwa muda.
Mitandao mingi kwa sasa inahamasisha juu ya ustawi, yakiwemo mafunzo ya yoga mtandaoni, kucheza, mazoezi ya viungo na mikutano kwa njia ya video mtandaoni kama sehemu ya kusaidia watu kuvuka nyakati hizi ngumu. Zitumie huduma hizi!
Usalama wa Kidijitali
J ihadhari na ongezeko la majaribio ya udukuzi katika kipindi hiki, yenye nia ya kukudanganya kutoa taarifa zako za siri au muhimu kwa mdukuzi kama vile taarifa za siri za akaunti zako, kudukuliwa vifaa vyako vya mawasiliano, kumtumia mdukuzi nywila zako, n.k kupitia viunganishi-wavuti feki vinavyotumwa na wadukuzi, dokyumenti za kidukuzi, jumbe na barua pepe za kidukuzi, n.k. Kuwa makini sana.
Ikiwa katika kipindi hiki mahali unapoishi inakulazimu kutotoka nyumbani, unaweza kutumia huduma za kununua na kuletewa chakula kwenye mtandao kupitia simu-janja. Zingatia kuwa baadhi ya hizi huduma huhitaji utumie programu ambazo zinasoma eneo ulilopo kupitia GPS yako. Ikiwa unaona hii ni hatari kwako, basi chagua njia mbadala ama piga simu moja kwa moja kwa watoa huduma za chakula ili uletewe badala ya kutumia programu hizi.
Linda WiFi yako: Tumia jina tofauti la WiFi yako ambalo halioneshi kwamba ni WiFi yako au chagua kuficha kabisa jina la WiFi yako. Iwekee WiFi yako nywila kuzuia mtu yeyote kujiunga na WiFi yako. Hakikisha nywila unayotumia ni ngumu. Ibadilishe nywila yako mara kwa mara. Pia badilisha nywila ya awali ya WiFi router yako na uzuie watumiaji wengine wa nje kujiunga na mtandao wako wa WiFi. Unaweza kufanya mabadiliko hayo yote ukishaingia kwenye WiFi router yako na kutafuta mtandaoni mwongozo wa jinsi ya kubadilisha nywila ya WiFi router yako.
Hakikisha vifaa vyako vya mawasiliano vina usalama wa msingi (kompyuta na simu): ni muhimu kuzingatia hili endapo utaanza kutumia vifaa vyako vya mawasiliano binafsi kwa kazi za kiofisi. Ni vema ukavichunguza vifaa vyako vya mawasiliano kama vipo salama kabla ya kuanza kuvitumia kwa kazi za kiofisi. Zingatia haya yafuatayo:
- Je, unatumia toleo jipya la mfumo wa uendeshaji wa program za kifaa chako cha mawasiliano (kwenye kompyuta na simu ulizonazo)?
- Futa programu zote ambazo si za muhimu/huzitumii (ikiwemo Flash na Java)
- Pakua matoleo mapya na yaliyoboreshwa ya mifumo ya uendeshaji wa programu kwenye vifaa vyako vya mawasiliano, pamoja na kupakua matoleo mapya ya programu zako
- Tumia antivirus kulinda vifaa vyako dhidi ya virusi (Kwa Windows tumia: Microsoft Security Essentials, na kwa mifumo mingine tumia Malwarebytes). Unaweza pia kutumia VirusTotal.com kukagua viambatanishia vya wavuti kabla ya kuvibonyeza au kuvifungua.
-
Fanya usanidi sahihi wa mfumo wa uendeshaji wa programu za kifaa chako - hii itategemeana na mfumo wa uendeshaji unaoutumia (kwa taarifa zaidi kuhusu mifumo mbalimbali, bonyeza viunganishi-wavuti vifuatavyo hapo chini), pamoja na:
-
Kufanya usimbuaji kamili wa diski (kwa mtumiaji wa MS Windows, tumia BitLocker au VeraCrypt kwa mtumiaji wa Mac OS tumia FileVault, kwa Linux tumia LUKS,
-
kwa watumiaji wa Android, nenda kwenye Settings> Security> Encrypt, kwa watumiaji wa vifaa vya iOS, vinasimbwa mara baada ya kuweka nywila/tarakimu).
-
Hakikisha unatumia nywila ngumu au tarakimu ndefu kwa usalama wa vifaa vyako vya mawasiliano, na pia hakiki usanidi wake (Windows, Mac)
-
Tumia vivinjari salama na vilivyoboreshwa kwaajili ya kuperuzi mitandaoni. Front Line Defenders tunapendekeza utumie Firefox (au Chrome au Chromium) na ukiongezee kivinjari chako usalama zaidi kwa kutumia: uBlock Origin, HTTPS Everywhere, Privacy Badger, Cookie AutoDelete, Facebook Container, na NoScript. Programu zote hizi hupatikana pia kwenye webstore ya kivinjari cha Chrome/Chromium.
Tumia programu ya kuhifadhi nywila zako salama mfano KeePassXC kutunza nywila zako nje ya mtandao (ikiwa utahitaji kutumia programu ya kuhifadhi nywila zako mtandaoni, tumia Bitwarden lakini hakikisha unasanidi 2-factor authentication kabla ya kuingia kwenye programu hii inayohifadhi nywila zako. Ila kumbuka kuwa, kuna hatari ya kuhifadhi nywila mtandaoni).
Ikiwa unahitaji kutumia programu ya uandishi inayokidhi mahitaji ya kiofisi, tumia LibreOffice.
Zingatia matumizi ya VPN au proxy kulinda taarifa zako mtandaoni dhidi ya mtoa huduma wako wa intaneti uwapo nyumbani. Ikiwa hautaki mtoa huduma wako wa intaneti kujua ni seva gani unayotumia, unaweza kununua VPN au kutumia moja kati ya hizi za bure:
- Baadhi ya VPN za bure: Psiphon, RiseUp VPN, Proton VPN, TunnelBear (yenye kikomo cha 500MB), Hideme (yenye kikomo cha 10GB), Hoxx, Speedify (yenye kikomo cha 2GB), Lantern (yenye kikomo cha 500MB), HolaVPN, Intra, Windscribe, SecurityKiss (yenye kikomo cha 9GB), Calyx VPN
- Baadhi ya VPN za kulipia: Express VPN, Mullvad, Tor Guard, Private VPN, ibVPN
Kufanyia kazi za ofisini nyumbani kutapelekea uwe unatunza taarifa za kiofisi (muda mwingine hata taarifa nyeti) kwenye vifaa vyako binafsi vya mawasiliano. Hivyo basi, amua ni vifaa gani utavitenga kwaajili ya kuhifadhia taarifa za kazi za kiofisi tu. Jiulize maswali kama:
- Je, ninapaswa kutumia simu yangu ya mkononi kwa kazi za kiofisi? Je, ninahitaji simu tofauti?
- Je, ninahitaji kompyuta tofauti?
- Ni nani mwingine zaidi yangu anayeweza kutumia vifaa vyangu vya mawasiliano ninavyotumia kwaajili ya kazi za kiofisi?
- Ninawezaje kutenganisha taarifa binafsi na zile za kiofisi?
- Je, ninapaswa kuunda akaunti mbili tofauti kwenye kompyuta yangu kwaajili ya matumizi ya kazi za kiofisi na ingine kwa shughuli za binafsi?
Panga ni kwa muda gani utahifadhi taarifa nyeti kwenye vifaa vyako binafsi vya mawasiliano. Je, utazihamishaje kwa njia salama?
Waweza kuwatumia watu taarifa zako kwa usalama zaidi kupitia huduma ya usimbuaji-wa-mwanzo-hadi-mwisho kwenye intaneti au kuitumia kutunza hizo taarifa zisiibwe. Mapendekezo ya huduma zingine ni pamoja na:
- Sync.com (yenye nafasi ya hadi 5GB bure)
- Mega.nz (yenye nafasi ya hadi 15GB free, ya bure)
- Ikiwa hautumii huduma ya usimbuaji-wa-mwanzo-hadi-mwisho, tumia programu ya Cryptomator kusimbua mafaili yako mwenyewe na kuhifadhi taarifa zako mtandaoni
- share.riseup.net nayo inaweza kukusaidia kutuma mafaili ya saizi hadi 50MB na ina usimbuaji-wa-mwanzo-hadi-mwisho. Hata hivyo, huduma hii huyafuta mafaili yako baada ya masaa 12.
- send.firefox.com inaweza kukusaidia kutuma mafaili ya saizi hadi 1GB na ina usimbuaji-wa-mwanzo-hadi-mwisho. Hata hivyo, huduma hii itafuta mafaili yako baada ya siku moja au baada ya kuyapakua mafaili yako mara moja. Unaweza kuzilinda taarifa zako zilizoko kwenye programu hii kwa kuweka nywila. Kuwa makini katika utunzaji wa nywila yako. Mfano: Waweza kujitumia kiunganishi-wavuti cha programu hii kupitia barua pepe, lakini ukajitumia nywila kupitia programu salama ya Signal.
- send.tresorit.com inaweza kukusaidia kutuma mafaili ya saizi hadi 5GB na ina usimbuaji-wa-mwanzo-hadi-mwisho. Hata hivyo, programu hii itafuta taarifa zako baada ya siku 7 au baada ya kuyapakua mafaili yako mara 10.
- OnionShare.org ni njia salama ya kutuma mafaili ya saizi yoyote moja kwa moja kutoka kwenye kompyuta yako kwa kutumia Tor Network.
Ni muhimu kufanya chelezo (backup) ya taarifa zilizoko kwenye vifaa vyako vya mawasiliano mara kwa mara (inashauriwa kufanya chelezo mara moja kwa wiki au baada ya kazi kubwa). Unaweza kutumia programu zinazopatikana katika mfumo wa kifaa chako (kama operating system backup option au FreeFileSync kwenye Windows, TimeMachine kwenye Mac, Déjà Dup kwenye Ubuntu).
Front Line Defenders inapendekeza kufanya chelezo ya data zako kwenye diski tofauti na ya ndani ya kompyuta yako mara kwa mara na kuificha diski yako. Njia nyingine ya kuhifadhi data zako salama ni kutumia huduma ya usimbuaji-wa-mwanzo-hadi-mwisho kwenye intaneti kama ilivyokwishaelezewa hapo awali, ingawa njia hii ina athari zake pia. Unapaswa pia kuifanyia simu yako chelezo ya data zake, tunapendekeza uhifadhi data za simu yako kwenye kompyuta kuliko kwenye intaneti.
Kufanya kazi za uandishi wa dokyumenti ukiwa mbali, kutakulazimu kushirikiana na wafanyakazi wenzako. Endapo utataka kuhariri dokyumenti yako kwa kushirikiana na wengine kwenye intaneti kupitia kivinjari chako, waweza kutumia programu kama:
- CryptPad - programu hii hulinda dokyumenti unayoihariri kwa kutumia usimbuaji-wa-mwanzo-hadi-mwisho. Unaweza kuhifadhi dokyumenti zenye ukubwa wa hadi 1GB, bure. Unaweza pia kujisajili bure kutumia huduma ya programu hii kuhifadhi dokyumenti zako bila ukomo (usipojisajili, dokyumenti zako zitafutwa baada ya miezi 3 kama hazijafanyiwa kazi).
- Riseup Pads - Programu hii hutumika kuhariri dokyumenti kwa kushirikiana na wengine kiurahisi. Waweza kusanidi ukomo wa kuhifadhi dokyumenti yako kwa mfano; hadi siku 1, siku 60 au mwaka mzima. Programu hii hutumia softiwea ya EtherPad.
Angalizo:
Huduma zote hizo mbili hapo juu zinaruhusu kila mtu unayeshirikiana naye kuhariri dokyumenti husika kutumia kuinganishi-wavuti ulichowatumia kubadilisha dokyumenti husika muda wowote! Hivyo basi, ni muhimu kulinda kiunganishi-wavuti cha dokyument husika.
Pia kuna program zingine za kulipia sawa na hizo hapo juu kama vile Google Docs na Microsoft Office 365.
Kufanya kazi ukiwa mbali pia kutakulazimu uhakikishe unawasiliana na wengine kwa njia salama. Tambua kuwa maongezi ya simu za mkononi pamoja na SMS hayako salama, na kampuni ya mtandao wa simu unayotumia inapata taarifa zako zote. Hivyo basi, kwa usalama wa mawasiliano yako, tunapendekeza utumie moja ya programu zifuatazo kama mbadala wa huduma za mitandao ya simu za mkononi:
- Signal: Ni programu inayotumia intaneti kutuma na kupokea jumbe fupi za maandishi na za sauti kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine, kupiga simu na kuwezesha mawasiliano ya kikundi. Kuboresha usalama zaidi wa mawasiliano yako, tunapendekeza ufanye usanidi ufuatao unapotumia Signal: Settings> Privacy> Screen lock, Screen Security and Registration lock. Pia tunapendekeza ufanyie usanidi meseji zako ziwe zinafutika baada ya muda flani kwa kubonyeza kitufe cha Disappearing Messages.
- Wire: Hutumia intaneti kutuma na kupokea jumbe fupi za maandishi na za sauti kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine, kupiga simu na kuwezesha mawasiliano ya kikundi. Unaweza kutumia anwani yako ya barua pepe ama namba yako ya simu kujisajili kutumia programu hii. Angalizo: Kwa sasa, Wire ni kampuni yenye maslahi ya kibiashara zaidi.
- Delta Chat: Pia hutumia intaneti kutuma na kupokea jumbe fupi za maandishi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine, pamoja na mawasiliano ya kikundi. Progamu hii huhitaji usajili wa anwani ya barua pepe ili uweze kuitumia.
Please see our Guide to Secure Group Chat and Conferencing Tools for recommendations on tools and advices on video calls, webinar or online training.
Utalazimika kuendelea kutumia anwani yako ya barua pepe ya kawaida. Zingatia usalama katika matumizi ya anwani yako ya barua pepe, kama vile kutumia nywila ngumu, kutumia uthibitisho wa mara mbili wa akaunti yako (2-factor authentication), kukagua usanidi wa anwani yako ya barua pepe kuhakikisha jumbe zako hazitumwi kwenda kwenye anwani zingine, ni vifaa gani vya mawasiliano vimeunganishwa na anwani yako ya barua pepe, nini kinaendelea kwenye akaunti yako ya barua pepe? – mara yako ya mwisho kuingia kwenye anwani yako ya barua pepe, n.k. Hata hivyo, ikiwa unahitaji kutengeneza anwani mpya ya barua pepe salama, Front Line Defenders inapendekeza utumie:
- Protonmail - ina uthibitisho wa mara mbili wa akaunti yako (nenda kwenye Settings> Security na ubonyeze two-factor authentication. Unahitaji kupakua programu ya andOTP, Duo Mobile au Authy kwenye simu-janja yako ili kukamilisha hatua hii na skanisha msimbo utaoonekana kwenye skrini ya kompyuta yako kwa kutumia programu hii).
Tutanota -huongeza uthibitisho wa akaunti yako mara mbili (nenda kwenye Settings> Login> Second factor authentication)
Zingatia kwamba, usalama wa barua pepe zako utakuwepo tu kati ya akaunti zinazotumia huduma hizi - Tutanota au Protonmail – zenye usimbuaji-wa-mwanzo-hadi-mwisho. Barua pepe ambazo hazitumii program hizi hazina usalama kama huu.
Ikiwa unahitaji kuchangia kalenda ya pamoja na wengine, tumia hizi:
Kwa mahitaji ya madodoso tumia:
- https://framaforms.org
- https://www.jotform.com
- https://tutanota.com/es/secure-connect (paid 50% discount for NGOs)
Tunakukumbusha kuwa mwangalifu kudhibiti taarifa nyeti katika matumizi ya huduma za kwenye intaneti.
Vifaa na programu za kufuatilia maendeleo ya afya za watu: Katika kipindi hiki, baadhi ya Serikali zimeweka utaratibu unaowataka wageni wanaoingia nchini mwao kupakua programu au kutoa namba za simu za mkononi ili waweze kukufuatilia afya za wageni. Hata hivyo, utaratibu huu unaweza kudumu muda mrefu kuliko kawaida. Wasiliana na mashirika ya ndege, Wizara za Mambo ya Nje au Balozi za nchi unayotaka kwenda, IATA na tovuti za mamlaka husika kabla ya kufanya uamuzi wa kusafiri. Ukiweza, tumia aina hiyo ya hizo programu kwenye Shelter app profile.
Miongozo ya ziada:
- How journalists can work from home securely - Freedom of the Press Foundation
- Digital Resilience in the Time of Coronavirus - Equality Labs
- How to Work From Home Without Losing Your Mind - Wired.com
- Remote Work and Personal Safety - Tor Project
- How to improve your digital safety while working remotely - SMEX
- GitLab's Guide to All-Remote - GitLab
- Community Resources for COVID19 - Internet Freedom Festival
Miongozo ya jumla ya Usalama wa Kidijitali:
- Security in-a-Box - Front Line Defenders and Tactical Technology Collective
- Surveillance Self-Defense - Electronic Frontier Foundation
- Digital First Aid Kit - Digital Defenders Partnership
- Security Planner - Citizen Lab
- Hygiene in Digital Public Square
- The Motherboard Guide to Not Getting Hacked